Na Dar es salaam news
KUPANDA kwa nauli za dadalala kiholela katika Kituo cha Makumbusho jijini Dar es Salaam pamoja na maeneo mengine,wananchi wanaotumia usafiri huo wametoa malalamiko yao na kuomba Mamlaka husika ikiwemo LATRA kuchukua hatua kudhibiti kupanda huko kwa nauli.
Kwa mujibu wa wananchi wa Makumbusho ambao wanapanda daladala katika Kituo cha Mabasi cha Makumbusho jijini Dar es Salaam wamesema madereva na makonda wa daladala wanapandisha nauli kiholela nyakati za usiku, hali inayowaweka abiria katika hali ngumu.
Tatizo hilo limezidi kuwa kubwa ambapo baadhi ya abiria wanalazimika kulipa mara mbili au zaidi ya nauli ya mchana, licha ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu (LATRA) kuweka wazi taratibu za nauli kwa usafiri wa umma, wasafirishaji wamekuwa wakipuuza taratibu hizi na kupandisha nauli bila kibali.
Hali hiyo ni kinyume na nauli rasmi zilizowekwa na mamlaka, na imekuwa njia ya madereva na makonda kujipatia kipato maradufu.
Kutokana na kupandishwa kwa nauli hizo wananchi wanalalamika kuwa jitihada za LATRA kudhibiti tatizo hilo zimeshindwa, hali inayowaacha wakiteseka na gharama kubwa za usafiri usiku.
Baada ya kuibuka kwa malalamiko hayo ya wananchi wa Makumbusho ,Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa LATRA Salum Pazzy amekiri kuwa wanapokea malalamiko na wanayafanyia kazi.
“Tunafanya hivi kuwarahisishia abiria kuweza kufikisha taarifa pale ambapo kuna changamoto na makosa kama hayo, yanapokuwa yamefika, tunafuatilia na tunafanya ukaguzi wetu mara kwa mara, wafanya makosa tunawachukulia hatua” amesema Pazzy.
Hata hivyo, Pazzy amesema kwa safari za mjini wameweka wasafirishaji wengi na idadi imekuwa kubwa,kiasi kwamba wakiongeza magari mengine watafanya mlundikano wa magari yasiyotoa huduma. Kwa mujibu wa tafiti wanazofanya kila mkoa, kupitia Ofisi ya Mfawidhi, wanaendelea kung’amua njia zipi zinauhitaji wa magari.
Amesema na wanahakikisha wasafirishaji wote wanaandika bei elekezi za nauli na namba ya huduma kwa wateja ubavuni mwa magari yao, kuwarahisishia abiria wenye changamoto kufikisha mahali husika na kushughulikiwa kwa wakati.
“Kama magari yanakuwa machache kiasi kwamba wanakaa muda mrefu, sasa unajua kila mtu anatafsiri yake, mtu anaweza kukuambia dakika 20 ni muda mrefu, mwengine nusu saa, muda mrefu” amesema Pazzy.
Pia ameeleza, wanaendelea kutoa ushirikiano kwa wadau, huku wakihamasisha na kutoa elimu kupitia vipindi vya runinga, mitandao ya kijamii,maonesho na sehemu mbalimbali.
Ili wasafirishaji wajue wajibu wao na abiria kujua haki zao za msingi kama kudai tiketi, kwani wasipofanya hivyo inawarahisishia wavunja sheria kupandisha bei za nauli.
“Muda wowote hata saa nane za usiku, jaribu kupiga namba ya Latra, alafu ripoti tatizo uone jinsi litakavyofanyiwa kazi, saa 24, hata saa tisa za usiku toa taarifa.
“Tutahitaji ujue namba ya gari iliyokufanyia makosa ya kuzidisha nauli, kama walikupa tiketi basi uwe na tiketi yako, kujua mamlaka inavyofanya kazi” amesema Pazzy.
ABIRIA WALALAMIKA
Kutokana na hali hiyo abiria wanaotumia Kituo cha daladala cha Makumbusho, walalamikia mamlaka husika kutokufanya kazi ipasavyo kwani wanaoumia ni wao wananchi, wakieleza sababu za kulipa nauli tofauti na iliyoandikwa kwenye tiketi, ingawa wengi wao wanaona bora kulipa nauli ambazo sio rasmi, kuliko kukaa muda mrefu kituoni.
Kelvin Makwinya, Mkazi wa Mbezi mwisho akitokea Makumbusho, amesema Dar es Salaam lazima nauli zipande, kwa sababu watu wanakuwa wengi sana katika kituo hicho na unaweza kukaa masaa mawili kituoni, hivyo inawalazimu kupanda magari yaliyokuwepo kwa wakati huo, wanayotoza nauli zaidi, ili kuwahi majumbani.
Pia abiria Ahmad Rashid, amesema foleni ndizo zinasababisha nauli kupanda, hasa ikifika nyakati za usiku, abiria ni wengi lakini magari ni machache kituoni.
“Sasa abiria anaona amekaa muda mrefu kituoni, yale magari ya ruti husika yamechelewa kufika, naye anataka kuwahi nyumbani kwa ajili ya kesho kuwahi kazini, kwaiyo unamkuta anaamua kupanda kwa shilingi 1000, ingawa sio nauli kamili” amesema Ahmad.
Othman Bonzo, mtu wa usalama wakujitolea katika Kituo cha Makumbusho, amesema mamlaka husika haitekelezi majukumu yake nyakati za usiku, maana magari yanayo pandisha nauli ni magari ya ruti tofauti.
Hii inasababishwa na uchache wa magari katika ruti hiyo. Pia amechagiza kwa kusema, hali hii ipo sehemu nyingi sio makumbusho tu.
“ Hizi gari za chuo, lakini zinaenda Makongo, hakuna gari ya Makongo inayopakia hadi saa mbili za usiku. Njia ya Makongo unakuta kwa siku ina gari moja” amesema Bonzo.
MADEREVA,MAKONDAKTA WAVUNJA UKIMYA
Kutokana na hali hiyo,baadhi ya makonda na madereva wameeleza mara nyingi wanaozidisha nauli kwa abiria nyakati za usiku, ni magari ya ruti tofauti yanayokuja kuingilia ruti husika.
Said Abubakari, msafirishaji abiria ruti ya Posta-Makumbusho amesema, wanaopandisha nauli nyakati za usiku ni makonda na madereva wenye tamaa na kusababisha kuharibu utaratibu uliowekwa na Latra.
“Madereva na makondakta wenyewe huwa wanachukulia kwa kuwa ni usiku, Latra wangekuwa wanafanya ukaguzi usiku, wangeshika magari mengi sana” amesema Said.
Ameendelea kwa kusema, Umoja wa Makonda na Madereva, hauna msimamo bali ni jina tu, wengi wao ni wanapiga hela, umoja huo ni maslahi kwa watu wachache tu.
Dereva wa daladala,Idris Abdul amesema changamoto za miundombinu ya barabara husababisha magari kutokufika kwa wakati katika vituo, hivyo abiria wengi hulundikana kwenye vituo.
Ameiomba Serikali kutengeneza miundombinu rafiki kwani wanakaa muda mrefu kwenye foleni, nakupelekea baadhi yao kutokukamilisha hesabu ya bosi kwa wakati, na kuwalazimu kupandisha nauli ili kufidia wakati waliopoteza kwenye foleni.
“Serikali na mamlaka zinazohusika, zichukue hatua zaidi kujaribu kuondoa hilo wimbi la foleni barabarani” amesema Idris.
CHAMA CHA KUTETEA ABIRIA WATOA NENO
Aliyekuwa Mwasisi na Mwenyekiti wa Chama cha Kutetea Abiria (Chakua), Hassan Mchanjama amesema suala la kupandisha nauli kiholela limekuwa changamoto kwa nyakati za usiku.
Amekiri mara kwa mara wamekuwa wakipokea malalamiko kutoka kwa abiria, kuhusu kupanda kwa nauli ikifika usiku, na wamejaribu kushirikiana na mamlaka bega kwa bega kutatua suala hilo.
“Changamoto iliyopo mamlaka kutokufanya kazi usiku ipasavyo, Latra wametoa leseni kwa muda, kwa mujibu wa kanuni na sheria za Latra , lakini usimamizi umekuwa changamoto” amesema Mchanjama.
Ameongeza kwamba kwa sasa wapo mbioni na kwenye hatua za mwishoni, ili kurudisha umoja huo, licha ya changamoto walizokutana nazo kabla ya kusimamishwa.
Amefafanua ikumbukwe Septemba, 2023 Chama hichi kiliacha kufanya kazi rasmi, kutokana na baadhi ya watu waliotumia nyaraka na vitambulisho vya chama, kujipatia kipato na si kutetea abiria.
Mchanjama, amesema wanendelea kufanya maboresho ya katiba ndani ya chama, na kubadili jina kuwa Taasisi ya Kutetea Haki za Abiria (Takuha). Wameiomba Serikali kuwaunga mkono kwani taasisi hiyo ni kwa maslahi ya wananchi.