Fikiria asubuhi unapoamka na kuvuta hewa safi ya asili, ukitazama majani ya kijani kibichi yakipepea kwa upepo mwanana. Fikiria maji ya mto yanayotiririka kwa amani, wanyama wa porini wakinywa maji, na watoto wakicheza kwa furaha bila woga wa magonjwa yanayotokana na uchafuzi wa mazingira. Mazingira haya tulivu na yenye afya yamekuwa sehemu ya maisha yetu kwa vizazi vingi, lakini je, tumejiuliza mara ya mwisho kama tutaweza kuyahifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo?
Kila siku, kasi ya mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa hewa, ukataji miti kiholela, na bidhaa zisizodumu zinatishia uhai wa mazingira yetu. Tunapuuza ukweli ambao upo kwenye mikono na macho yetu katika kuharibu maisha yetu wenyewe, kwamba kila tunachofanya leo kina athari za moja kwa moja na za muda mrefu kwenye hewa tunayovuta, maji tunayokunywa, na ardhi tunayolima. Sasa ni wakati wa kuamka na kuchukua hatua — kulinda na kuheshimu haki na wajibu wetu wa kimazingira.
Kusimama na kulinda mazingira si jukumu la serikali tu; ni jukumu la kila mmoja wetu. Kupitia makala hii, tutachunguza jinsi haki na wajibu wa kimazingira zinavyohusiana na afya yetu, uchumi wetu, na mustakabali wetu. Ni wakati wa kuungana na kuchukua hatua kwa ajili ya mazingira, kwa sababu tukiyaharibu leo, hakuna kesho yenye hewa safi na ardhi yenye rutuba.
Katika jamii ya sasa, haki na wajibu wa kimazingira ni dhana inayojenga msingi wa maisha bora na maendeleo endelevu. Kwa maana mazingira yanayozungumzwa ni pamoja na hewa tunayovuta, ardhi tunayolima, maji tunayokunywa, na viumbe hai wanaotuzunguka. Ni jukumu letu sisi kama binadamu pamoja na serikali kuhakikisha tunalinda haki za kimazingira kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Nini Sababu ya Mambo Haya Kutokea?
Haya ni machache kati ya mengi:
1. Matumizi ya Bidhaa za Muda Fupi za Viwandani
Katika miaka ya hivi karibuni, viwanda vimeongeza uzalishaji wa bidhaa fupi ambazo haziwezi kudumu muda mrefu. Mfano ni mavazi yaliyotengenezwa kwa malengo ya matumizi ya muda mfupi na mara nyingi hutupwa baada ya muda mfupi. Mavazi kama haya yasiyodumu husababisha kuongezeka kwa takataka, uchafuzi wa mazingira na hatari kwa jamii. Kwa upande mwingine, mavazi yanayolenga kuonyesha sehemu za mwili wazi yamechangia kwa kiasi fulani kuongezeka kwa matukio ya unyanyasaji wa kijinsia, jambo ambalo ni tishio kwa usalama wa wanawake na watoto katika jamii zetu.
2. Uzalishaji wa Chakula Kupitia Teknolojia
Leo, ufugaji na kilimo vimebadilika na teknolojia mpya imesaidia kuharakisha ukuaji wa wanyama na mimea, lakini kwa gharama ya afya ya walaji. Kuku wanaokuzwa kwa muda mfupi kwa kutumia dawa kali wanaweza kuwa na madhara kwa mlaji. Vilevile, wakulima wa mbogamboga hutumia kemikali nyingi ili kuzuia wadudu waharibifu, lakini mara nyingi wanauza bidhaa hizo kabla ya muda wa dawa kuisha, jambo ambalo linaweza kusababisha magonjwa kama saratani na kisukari.
3. Ujenzi na Ukosefu wa Mipango Endelevu
Kasi ya ujenzi mijini imekuwa kubwa, huku maeneo mengi miti inakatwa na kuacha maeneo wazi bila kupandwa miti upya. Hali hii inasababisha ongezeko la joto na ukosefu wa hewa safi. Miti ina faida kubwa kwa afya ya binadamu. Hapa kuna orodha ya magonjwa yanayoweza kusababishwa au kuzidishwa na ongezeko la joto:
- Kiharusi cha joto (Heat Stroke) – Hali inayotokea pale mwili unaposhindwa kudhibiti joto, ikisababisha joto la mwili kupanda na kusababisha kizunguzungu, maumivu ya kichwa, kichefuchefu, na hali mbaya zaidi inaweza kusababisha kifo.
- Mshtuko wa joto (Heat Exhaustion) – Hali inayotokana na mwili kupoteza maji na chumvi kwa kasi kupitia jasho, na kusababisha dalili kama vile kizunguzungu, uchovu, kichefuchefu, na maumivu ya kichwa.
- Magonjwa ya ngozi kama vile Upele wa joto (Heat Rash) – Hali ya ngozi yenye upele unaowasha, hutokea zaidi kwa watoto wadogo na watu wanaotumia muda mrefu katika maeneo yenye joto kali.
- Magonjwa ya moyo na mishipa (Cardiovascular Diseases) – Joto kali huongeza mzigo kwenye moyo, hususan kwa watu wenye matatizo ya moyo, na inaweza kusababisha shinikizo la damu na mshtuko wa moyo.
- Dehydration – Mwili unapopoteza maji mengi kwa njia ya jasho, mtu anaweza kukosa maji mwilini, hali inayoweza kusababisha matatizo ya figo, shinikizo la damu, na kushindwa kufanya kazi vizuri.
- Msongo wa mawazo na magonjwa ya akili (Mental Health Issues) – Joto kali linaweza kuchangia msongo wa mawazo, usingizi usio na utulivu kiakili kama wasiwasi na mfadhaiko.
- Magonjwa ya mfumo wa kupumua (Respiratory Illnesses) – Joto kali linaweza kuzidisha hali ya magonjwa kama pumu, hasa maeneo yenye uchafuzi wa hewa wa hali ya juu.
- Magonjwa ya maambukizi ya njia ya mkojo (UTI) – Ongezeko la joto linaweza kuchangia kuongezeka kwa maambukizi ya njia ya mkojo, kwani watu hukosa maji mwilini na hivyo hupunguza mkojo.
- Saratani ya ngozi (Skin Cancer) – Joto linaenda sambamba na mionzi ya jua yenye nguvu, ambayo inaweza kuharibu ngozi na kuongeza hatari ya kupata saratani ya ngozi.
- Maambukizi yanayohusiana na maji (Waterborne Diseases) – Joto kali linaweza kuchangia kuenea kwa magonjwa yanayoambukizwa kupitia maji, kama kipindupindu, hasa kwenye maeneo yenye maji yaliyosimama na yasiyosafishwa vizuri.
Ni muhimu kuweka vivuli na nafasi za kujipatia hewa safi kwa abiria wanaosubiri usafiri hususani barabarani. Fanya safari kutoka kituo kimoja cha daladala kwa mguu au gari uone namna ambavyo miti ilivyoadimika. Vituo vya abiria vinapaswa kuzingatiwa kwa kuweka miti na mimea ili kupunguza joto na kusaidia usafi wa hewa. Kwa nini uwe mteja mtarajiwa kwenye hospitali? Unaweza kuepuka gharama hizi kwa kupanda miti katika maeneo yetu ya makazi, weka mbali karo la maji taka na kisima cha maji ya matumizi mbali ili kuepuka kunywa uchafu.
4. Uchafuzi wa Ardhi na Maji
Kutokuwepo na udhibiti wa maeneo ya gereji za magari mijini na vijini kumesababisha uchafuzi wa ardhi kutokana na kumwagwa kwa mafuta na kemikali nyingine ambazo ni hatari kwa afya ya jamii na viumbe wa ardhi. Serikali inapaswa kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya gereji ili kuzuia uchafuzi wa ardhi na maji, hatua ambayo itaboresha hali ya mazingira na kulinda afya za wakazi wa maeneo ya karibu.
ANGOZA: Nini Serikali na Jamii Zifanye?
Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha sheria na sera zinazohakikisha haki za kimazingira zinalindwa. Ni muhimu kutunga sheria zitakazoweka udhibiti mkali kwa viwanda, kufuatilia ubora wa chakula, na kuhimiza kilimo na ufugaji unaofuata njia za asili angalau kwa asilimia 80%. Pia, elimu kwa jamii ni muhimu ili watu waweze kuelewa wajibu wao katika kulinda mazingira. Serikali ya Zanzibar iweke nguvu kwenye hii program ya GREEN LEGACY kwa kuziwezesha asasi za kiraia kuzipatia miradi ambayo itasaidia upandaji miti kwa kiasi kikubwa. Kwa mfano, Jozani Environmental Conservation Association (JECA) imeweza kupanda miti 30,000 kwa mwaka mmoja. Pia kuanzisha kampeni za upandaji miti na kuhamasisha uhifadhi wa mazingira kwa kila mtu.
Kwa pamoja, serikali na jamii zinaweza kushirikiana ili kulinda na kuhifadhi mazingira. Ni haki yetu kuwa na mazingira safi na salama. Afya kwa Jamii – ANGOZA chini ya ufadhili wa commonwealth umeendesha mafunzo kwa jumuiya 50 kwa Zanzibar juu ya Haki na Wajibu wa Kimazingira: Uangalizi wa Mazingira Yetu kwa Afya ya Jamii na Maendeleo Endelevu