Na Heri Shaban, dar es salaam news
DIWANI wa viti Maalum Wanawake wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam Magreth Cheka ,ambaye ni Mlezi wa Kata ya Kivule amewataka Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika Kata hiyo kuunda vikundi vya Wanawake kwa ajili ya kupata mikopo ya Serikali ambayo inatarajia kufunguliwa rasmi julai mwaka huu.
Akizungumza katika mkutano wa UWT tawi la Mji Mwema Kata ya Kibule amesema anawaomba wanawake wa UWT Kivule kuunda vikundi vya wanawake kwa ajili ya mikopo ya Serikali ili wajikwamue kiuchumi.
“Hivi karibuni mikopo hiyo itatoka rasmi hivyo kila kikundi cha mkopo kifuate taratibu ikiwemo kujisajili katika mfumo wa mtandao ukiwa na vitamburisho vya NIDA,”amesema Cheka na kuwataka wanawake hao kushirikiana na Mama Maendeleo wa Kata kwa ajili ya kupewa elimu ya usajasiriamali na taratibu za usajili wa kisasa .
Pia amewataka makatibu wa vikundi vya vikoba kushirikiana na Ofisa Maendeleo ya Kata ya Kivule kwa ajili ya mchakato wa kusajili vikundi vyao ili viwe katika taratibu za kupata mikopo hiyo ya asilimia kumi ambayo inatoleqa ngazi ya Halmashauri zote nchini .
Amesema mikopo ya Serikali aina riba hivyo wachangamkie fursa ya kukopa ili wakuze mitaji yao sambamba na kufanya marejesho katika taasisi za Benki ambazo watapangiwa kuchukua mikopo hiyo na taratibu wataelezwa .
Aidha alitaka kila wanawake wa vikundi vya mkopo kufamiana ili kuondoa usumbufu wakati wa marejesho.
Kwa upande wake Katibu wa UWT Mji Mwema Kivule jijini Dar es Salaam Sarah Isesha amesema tawi la UWT Mji Mwema lina wanawake wa UWT 260 wanachama wa CCM 270 kati yao wenye kadi za mpiga kura 143 na wenye namba za NIDA 140 mikakati yao kuongeza wanachama kufikia 500 .
Amesema mikakati yao mingine UWT Mji Mwema ni kuongeza wanachama na wakusajili katika mfumo wa kadi za kisasa la kieletroniki.