Na Dar es Salaam news
WAKAZI wa jijini Dar es Salaam na hasa waliopo katika barabara ya Nyerere wamekuwa wakishuhudia ujenzi wa barabara ya mabasi ya mwendokasi inayoendelea kujengwa kwa kasi huku baadhi yao wakimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kutoa fedha kufanikisha ujenzi huo.
Ujenzi wa barabara ya mwendo kasi pamoja na kusababisha msongamano wa magari katika baadhi ya maeneo kutokana na ujenzi huo bado mioyo ya wakazi wa maeneo hayo wameonesha kuufurahia kwani wanaamini utakapokamilika unakwenda kuondoa changamoto ya usafiri.
Katika Jiji la Dar es Salaam wakazi wa Gongolamboto na maeneo jirani wanaotumia barabara ya Nyerere wanatamani kuona barabara inakamilika na mabasi ya mwendo kasi yanaanza kusafirisha wakazi hao wanaotumis barabara hiyo kwenda na kurudi katika shughuli zao za kila siku.
Wakizungumza na Dar es Salaam news baadhi ya wakazi wakiwemo wa Uwanja wa Ndege,Karakata, Majumbasita, Banana,Ukonga, Mombasa , Gongolamboto kuelekea Chanika wamesema wanachofurahia ni kuona kila siku kumekuwa na mabadiliko ya ujenzi,kwani mkandarasi anaendelea na ujenzi kwa kasi inayoridhisha.
Shaban Mussa mkazi wa Banana na Joyce Chuma wa Mombasa wanaeleza kuwa Moja ya changamoto waliyonayo ni uhaba wa daladala vituoni hivyo kusababisha kutumia muda mwingi vituo vya mabasi,hivyo ujenzi utakapokamilika ba huduma kuanza hakutakuwa na changamoto hiyo tena.
“Maeneo ambayo wanatumia mabasi ya mwendo kasi hawana shida tena ya usafiri, wanakwenda vituoni na kuingia kwenye basi na kisha kwenda katika shughuli zao .Tunakumbuka enzi zile Kimara hawana mwendo kasi waliteseka sana na leo wamesahau.Hivyo nasi tunaelekea huko .Acha wajenge na sisi tunasubiri kwa hamu.
“Hivyo na sisi wa barabara hii ya Nyerere tunakwenda kunufaika na kuboreshaji wa miundombinu unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.Tunamshukuru Rais na Serikali yake kwa kuona umuhimu wa kuboresha miundombinu ya barabara inayoendana na mahitaji ya sasa,”amesema mkazi Shaban Mussa.
Wakati wakazi hao wakisubiria kwa hamu barabara ya mwendokasi ,tayari Wakala wa Barabara Tanzania(TANROAD) Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa ukitoa taarifa mbalimbali kuhusu uboreshaji wa miundombinu ya barabara na hasa ya mwendokasi
KAULI YA RC CHALAMILA
Wakati akikagua barabara hiyo kwa nyakati tofauti alipokuwa akikagua barabara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila alisema barabara ya Nyerere inayotokea mjini hadi Gongo la Mboto Ina urefu wa kilometa 23.3 na barabara hiyo ni muhimu kwa uchumi wa nchi yetu.
Vilevile ni ya Kidiplomasia ni barabara inayoelekea uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, hivyo Rais Dkt Samia Suluhu Hassan anataka kuona barabara hiyo inaisha mapema na ikiwezekana hata kabla ya muda uliowekwa kwa mujibu wa mkataba ili kufungua fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Barabara hiyo inayojengwa na mkandarasi Sino Hydro kwa mujibu wa Chalamila ni kwamba ni vema ujenzi wake ukamilike kwa wakati.
Pamoja na maelezo hayo Mkuu wa Mkoa Chalamila amesema Rais Dk.Samia amekuwa akifanya maboresho makubwa ya miundombinu katika Mkoa wa Dar es Salaam na dhamira yake ni kuona maboresho ya miundo mbinu yanafungua fursa ya watu kufanya biashara saa 24 na sio saa 12 kama ilivyo sasa ukizingatia Dar es Salaam ni jiji la kibiashara.
Kwa habari zaidi na matukio yanayoendelea, endelea kufuatilia daressalaamnews.co.tz, share na uwapendao kwa habari hizi muhimu.